MZITO
ANA KILO NGAPI?
Nafungua ukurasa, kuyasema waziwazi,
Maneno haya ya sasa, naomba kumaizi,
Hata pale kwenye misa, wanatajwa kama kazi,
Na huyu mtu mzito, huwa ana kilo ngapi.
Taraa mimi natamba, ninapagazwa mzito,
Ninapompiku simba, mzito kwangu ni kito,
Kwangu waja kujibamba, wakinisifu mzito
Na huyu mtu mzito, huwa ana kilo ngapi.
Napata hurulaini, mrembo mwenye ulimbo,
Tunaenda maskani, nalifurahia pambo,
Ninahisi huru ndani, mzito mwenye mrembo,
Na huyu mtu mzito, huwa ana kilo ngapi.
Salamu barabarani, kilo zaniongezeya,
Zasemwa kwa burudani, vipi mzito mseya,
Ninatoswa tamashani, mzito naposikiya,
Na huyu mtu mzito, huwa ana kilo ngapi.
Kigezo chake uzito, niambieni wangwana,
Nkijilipia koto, jina mzito lafana,
Yule aliwasha moto, mzito mwamwita bwana,
Na huyu mtu mzito, huwa ana kilo ngapi.
Kijana mkware
yule, yeye pia ni mzito,
Anapolowea mle, anazua tumbo joto,
Na hamtoi kelele, sababu yeye mzito,
Na huyu mtu mzito, huwa ana kilo ngapi.
Ninashindwa kueleza, uzito wa neno hili,
Nani kwenu anaweza, kunipatia fasili,
Nipeni ya kupendeza, nijuwe nisiwe nili,
Na huyu mtu mzito, huwa ana kilo ngapi.
Labaan
Shabaan
Sultani
Msudani
Malenga
Wa Turkana





